Kwa nini,Namibia imevunja mkataba na Wamarekani ghafla matumizi ya AI na Satelaiti katika kilimo?

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Namibia imesitisha mkataba wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 2.4 (takriban Shilingi bilioni 6.6 za Kitanzania) kati ya Wizara ya Kilimo na Kampuni ya 6th Grain Corporation inayojihusisha na teknolojia ya kilimo kutoka nchini Marekani.
Picha na Mtandao.

Mkataba huo ulihusu utumiaji wa mifumo ya Akili Unde (AI) na picha za satelaiti kwa ajili ya kufuatilia na kukadiria mwenendo wa uzalishaji wa mazao nchini humo.

Uamuzi huo wa ghafla umetangazwa na Msemaji wa Wizara ya Kilimo, Maji na Mageuzi ya Ardhi ya Namibia, Romeo Muyunda.

Ameeleza kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya ukaguzi wa kina wa kisheria kubaini kuwa,makubaliano hayo yalighubikwa na ukiukaji mkubwa wa taratibu za kiserikali na sheria za ununuzi wa umma.

"Uchunguzi wa kimkataba uliobuniwa na wizara ulijiridhisha bila shaka kuwa makubaliano hayo hayakukidhi vigezo vya lazima vya kisheria na kiutaratibu vinavyoongoza mikataba yote inayofanywa kwa niaba ya serikali kuu,"amesema Muyunda wakati akifafanua sababu za kuvunjwa kwa ushirikiano huo.

Chini ya mkataba huo uliopewa jina la Remote Sensing Agricultural Services Agreement, Kampuni ya 6th Grain Corporation ilitakiwa kuweka mifumo ya kidijitali inayotumia data za anga (satellite imagery) kutambua afya ya mimea, kukadiria kiasi cha mavuno ya kimkakati kama mahindi na mtama na kutoa tahadhari za mapema dhidi ya majanga ya tabianchi.

Hata hivyo, kabla ya hatua hii ya kisheria, mradi huo ulikuwa umeanza kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wataalamu wa usalama wa mtandao na wachambuzi wa masuala ya chakula nchini Namibia.

Hoja kuu ilikuwa ni "Utawala na Ulinzi wa Data za Kitaifa" (Data Sovereignty). Walidai kuwa kuipa kampuni ya kigeni mamlaka kamili ya kukusanya, kuchakata na kumiliki kanzi-data (database) ya rasilimali za chakula za nchi kunahatarisha usalama wa taifa na kujenga utegemezi wa kiteknolojia.

Aidha,wachambuzi wa masuala ya kijiografia na kiuchumi katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) wanaona hatua hii kama kengele ya heri kwa mataifa yanayoendelea.

Pia,inasisitiza umuhimu wa kuwekeza kwenye mifumo ya ndani ya kiteknolojia (local digital infrastructure) na kulinda data za sekta ya uzalishaji.

Hatua hii inakuja wakati ambapo mataifa ya ukanda huo, ikiwemo Tanzania yapo kwenye mapinduzi makubwa ya kilimo cha kidijitali.

Serikali zinashauriwa kuhakikisha kuwa sheria za ununuzi wa umma zinazingatiwa kikamilifu na wataalamu wa ndani wanashirikishwa ili kuzuia hasara za kifedha na uvujaji wa taarifa nyeti za kiuchumi kupitia mikataba ya kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here