NA DIRAMAKINI
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro ametangaza kuwa, vikao vya chama hicho vilivyokutana jijini Dar es Salaam vimepitisha kwa kauli moja jina la Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao husika vya CCM kujadili na kuridhia jina la Mhe. Ndejembi, ambaye ni mwanachama wa chama hicho ili kujaza nafasi ya Makamu wa Rais iliyo wazi kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo,Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Balozi Dkt. Migiro amesema, mchakato huo umefanyika kwa kuzingatia taratibu za ndani ya chama, hatua inayofungua njia kwa jina la Mhe. Ndejembi kuwasilishwa mbele ya Bunge kwa ajili ya kuthibitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Iwapo atathibitishwa na Bunge, Mhe. Ndejembi ataingia katika nafasi hiyo na kuchukua majukumu yanayotokana na Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa mujibu wa Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Ndejembi anatekeleza majukumu ya Waziri wa Nishati, nafasi ambayo imempa dhamana ya kusimamia sera, mipango na utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika sekta ya nishati nchini.
Katika wadhifa huo, amekuwa akihusika na masuala yanayohusu uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha sekta ya nishati na kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.
Uamuzi wa CCM unafungua hatua inayofuata katika mchakato wa kumpata Makamu wa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya jina la Mhe. Ndejembi kuwasilishwa rasmi Bungeni, wabunge watatakiwa kulithibitisha kwa mujibu wa masharti ya Katiba.
Aidha,endapo atapata idhini ya Bunge, taratibu nyingine za kikatiba zitakamilishwa, na hivyo kuwezesha uteuzi wa Makamu wa Rais mpya kuchukua mkondo rasmi.
Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo mbalimbali ya kitaifa, huku nafasi ya Makamu wa Rais ikiwa sehemu muhimu ya muundo wa uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nchimbi afukuzwa uanachama CCM
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro ametangaza kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi amefukuzwa uanachama wa CCM.

Katibu Mkuu huyo amesema, vikao hivyo vilijadili tuhuma za ukiukwaji wa maadili, kanuni na misingi ya CCM, ambapo baada ya suala hilo kuchunguzwa na kujadiliwa na vyombo husika, vikao vilifikia uamuzi wa kumfukuza uanachama.
Dkt.Migiro amesema,vikao hivyo vilibaini kuwa, baadhi ya matendo ya Dkt. Nchimbi hayakuendana na misingi, nidhamu na maadili yanayoongoza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
Amesema,uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa taratibu na kanuni za CCM, ukiwa na lengo la kulinda nidhamu, uadilifu na misingi ya chama, na si kumlenga mtu binafsi.
Tags
Breaking News
Chama Cha Mapinduzi
Deogratius Ndejembi
Habari
Mgombea Makamu wa Rais
Uteuzi wa Makamu wa Rais
