NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amempongeza Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi kwa kuapishwa na kuanza rasmi majukumu yake mapya ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiahidi ushirikiano katika kuhakikisha Serikali inatekeleza kwa ufanisi ahadi zake kwa Watanzania.
Mheshimiwa Kikwete ametoa ujumbe huo wa pongezi akieleza kuwa,kuapishwa kwa Ndejembi ni hatua muhimu katika safari yake ya kulitumikia Taifa na kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kutekeleza ahadi zilizoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kupitia ujumbe wake,Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amesema,yeye binafsi pamoja na Menejimenti nzima ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wanamtakia Mheshimiwa Ndejembi kila la heri na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
“Salamu nyingi za pongezi na dua njema kwako, Mheshimiwa Deo Ndejembi, katika siku hii muhimu unapoapa kuanza kazi kubwa ya kuisaidia nchi yako na kumsaidia Mheshimiwa Rais kutimiza ahadi zake za Ilani kwa Watanzania,”amesema Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.
Amesema, ofisi hiyo iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Makamu wa Rais Ndejembi katika kutekeleza majukumu yake, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
“Ahadi yetu ni ushirikiano mkubwa na kuchapa kazi kwa kiwango kikubwa sana,”amesema Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.
Makamu wa Rais Ndejembi ameanza rasmi majukumu yake mapya baada ya kuapishwa leo Agosti 29,2026 Ikulu Chamwino jijini Dodoma huku akitarajiwa kushirikiana na viongozi na watendaji wengine wa Serikali katika kusukuma mbele utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa manufaa ya Watanzania.
Ujumbe wa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete umehitimishwa kwa kaulimbiu #KaziNaUtu na #KaziIendelee, zinazosisitiza umuhimu wa uwajibikaji,mshikamano na kuendelea kutumikia Taifa kwa bidii.
Tags
Deogratius Ndejembi
Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania
Ofisi ya Rais-Utumishi
Ridhiwani Kikwete

