NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 24 Agosti, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Diaspora ya Afrika (ADDI), Balozi Arikana Chihombori-Quao, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania, ADDI na diaspora ya Afrika katika kuchochea maendeleo ya Bara hilo.
Viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuwawezesha vijana kuielewa historia ya Bara la Afrika, nafasi yao katika maendeleo na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi duniani.
Rais Dkt. Samia amesema, vijana wanahitaji maarifa yatakayowawezesha kuelewa mazingira ya sasa ya dunia na kushiriki kikamilifu katika kujenga mustakabali wa nchi zao na Afrika kwa ujumla.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwafundisha vijana uzalendo na kuwajengea uelewa wa masuala ya uraia, uongozi, matumizi sahihi ya habari na ushiriki katika shughuli za kijamii na maendeleo.
Mazungumzo yao pia yamegusia nafasi ya wanawake katika malezi, ujenzi wa jamii, uongozi, uhifadhi wa utamaduni na kuendeleza maarifa ya asili ya Bara la Afrika.
Kwa upande wake, Balozi Chihombori-Quao amempongeza Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake na hatua za maendeleo zinazoendelea kutekelezwa nchini.
Amesema ushirikiano kati ya Afrika na taasisi yake una nafasi muhimu katika kuhamasisha uwekezaji, kuunganisha maarifa na kujenga mtazamo chanya kuhusu Bara hilo.
Rais Dkt. Samia amempongeza Balozi Chihombori-Quao kwa juhudi zake za muda mrefu za kutetea maslahi ya Afrika na kuimarisha uhusiano kati ya Bara hilo na watu wenye asili ya Afrika wanaoishi nje ya Bara.
Tags
Africa Development
African Diaspora Development Institute (ADDI)
Afrika
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Kimataifa



