UMOJA wa Falme za Afrika umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Tanzania kwa kutumia utaalamu wa majaji kutoka nchi nyingine za Afrika katika Tume ya Uchunguzi kuhusu matukio yaliyozunguka Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Umoja huo umesema hatua hiyo inaweza kuimarisha uwazi, weledi, uadilifu na imani ya wananchi katika mchakato wa uchunguzi.Katika taarifa yake ya Agosti 11, 2026, Umoja huo umesema Afrika ina wataalamu wenye uzoefu katika sheria, haki za binadamu, haki, utawala na utatuzi wa migogoro.
Umesema utaalamu huo unapaswa kutumika kuimarisha uchunguzi badala ya kutafsiriwa kuwa ni kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Umoja huo umesema ushiriki wa majaji kutoka nchi nyingine haupaswi kuchukuliwa kama udhaifu wa mfumo wa haki wa Tanzania.
“Badala yake, inaweza kuonekana kuwa ni dhihirisho la kujiamini, ukomavu wa taasisi na utayari wa kuruhusu mitazamo mbalimbali ya kisheria na uzoefu wa kitaalamu kuchangia katika suala lenye umuhimu wa kitaifa,” umesema.
Umesema nchi za Afrika zinapaswa kusaidiana katika kuimarisha haki, amani na utawala wa sheria, huku ukisisitiza kuwa mipaka ya kisiasa haipaswi kuzuia ushirikiano wa kitaalamu.
Umetaja Tanzania, Afrika Kusini, Malawi, Namibia na Uganda kuwa na historia ya ushirikiano katika amani, maendeleo, demokrasia na utawala bora.
Umesema ushiriki wa majaji kutoka Namibia na nchi nyingine za Afrika unaweza kuimarisha mshikamano wa bara na ushirikiano wa kitaalamu.
“Tunapaswa kujitahidi kujenga Afrika ambayo wataalamu wanaweza kuvuka mipaka ya kitaifa kuchangia utaalamu wao pale ujuzi wao unapohitajika, bila ushirikiano huo kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ni kuingilia mamlaka ya nchi nyingine,” umesema.
Umoja huo pia umesema ushiriki wa wataalamu kutoka mataifa mengine unaweza kuongeza imani ya wananchi katika mchakato huo.
Hata hivyo, umeeleza kuwa Tume inapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, masharti yake na mamlaka iliyopewa.
Umesema kuwepo kwa jaji kutoka nchi nyingine hakupaswi kuchukuliwa kuwa tatizo lenyewe, kwa kuwa majaji hao wanaweza kuleta mitazamo mipana na uzoefu wa mifumo mingine ya sheria.
Umoja huo umewataka wadau kuipa Tume nafasi ya kukamilisha kazi yake kabla ya kufikia hitimisho kuhusu uaminifu au matokeo ya uchunguzi.
Pia umesema jaji anayeshiriki anapaswa kuheshimiwa kwa weledi na kuruhusiwa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru bila ushawishi usiofaa.
Umoja huo umesema haipaswi kuwepo dhana kwamba majaji wa Afrika hawawezi kushirikiana kuvuka mipaka katika masuala ya haki, uwajibikaji na utawala wa sheria.
Umesema matukio ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 yameibua maswali yanayohitaji majibu ya kuaminika na umeunga mkono jitihada za kupata ukweli.
Umetaka uchunguzi huo uongozwe na ukweli, haki, uwazi na maslahi ya Watanzania wote bila kujali msimamo wa kisiasa au nafasi ya mtu katika taasisi.
Pia umesema mchakato huo unapaswa kusaidia kuimarisha umoja wa kitaifa, imani ya wananchi kwa taasisi na njia za amani za kushughulikia malalamiko.
Umoja huo umewataka wadau wa Afrika na kimataifa kuunga mkono jitihada za kupata ukweli kuhusu matukio yenye utata na kuimarisha taasisi zinazoshughulikia changamoto kwa njia za kisheria na za amani.
Umesema ushiriki wa majaji kutoka Namibia, Uganda na nchi nyingine za Afrika unapaswa kuonekana kama fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda na imani ya wananchi katika jitihada za kupata ukweli.
“Tanzania ni jirani yetu, Tanzania ni dada na kaka yetu, na amani na utulivu wa Tanzania ni sehemu ya amani na utulivu wa Afrika yetu,” umesema.