NA DIRAMAKINI
NYUMBA za Upataji Nafuu maarufu kama Sober Houses, ni miongoni mwa mazingira salama na rafiki yanayoweza kuwasaidia watu wanaopambana na utegemezi wa dawa za kulevya katika safari ya kuacha matumizi ya dawa hizo na kurejea katika maisha ya kawaida.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), mazingira hayo yana umuhimu katika kuwapatia waathirika wa matumizi ya dawa za kulevya nafasi ya kuendelea na mchakato wa kuimarika baada ya kupata huduma za matibabu na urekebishaji wa tabia.
Nyumba za aina hiyo huweka mazingira yanayosaidia kujenga nidhamu, uwajibikaji na mshikamano miongoni mwa wanaopitia hatua ya kupona.
Pia, ni sehemu ya kuwasaidia kurejea katika shughuli za kijamii na kiuchumi bila kukumbwa kwa urahisi na vishawishi vinavyoweza kuwasukuma kurejea katika matumizi ya dawa za kulevya.
DCEA imeendelea kuhimiza jamii kuwa na mtazamo chanya kwa watu wanaopitia changamoto ya utegemezi wa dawa za kulevya, badala ya kuwanyanyapaa. Msaada wa familia, marafiki na jamii kwa ujumla ni muhimu katika kuwawezesha waathirika kuendelea na safari yao ya kupona.
Vilevile,jamii inahimizwa kushirikiana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa msaada kwa waathirika, kuzuia matumizi miongoni mwa vijana na kuendeleza mazingira yanayowezesha watu waliopona kurejea katika maisha yenye tija.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
Nyumba za Upataji Nafuu
Sober House
