Tume ya Jaji Lila ipo kisheria na inatekeleza jukumu tofauti na ile ya Jaji Chande,ipewe ushirikiano-Wakili Nkuba

NA GODFREY NNKO

WAKILI Msomi Sweetbert Nkuba kutoka Kampuni ya Sweet and Conrad amesema,Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 inayoongozwa na Jaji mstaafu Shabani Ally Lila imeanzishwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania, hivyo wananchi na wadau wote wanapaswa kuipa ushirikiano ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Wakili Nkuba ameyasema hayo leo Agosti 11,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uhalali wa tume hiyo na utofauti wake na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 iliyoongozwa na Jaji mstaafu Othman Chande.

Amesema,mamlaka ya Rais ya kuunda Tume za Uchunguzi inatokana na Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Sheria ya Uchunguzi,Sura ya 32 ya Sheria za Tanzania.

Kwa mujibu wa Wakili Nkuba, mamlaka hayo yanamwezesha Rais kuanzisha Tume ya Uchunguzi pale anapoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo, kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria zinazohusika.

“Kwa hiyo,Tume hii mpya ya Uchunguzi wa Kijinai au Tume ya Jaji Shabani Lila, uhalali wake kama ilivyokuwa Tume ya Jaji Chande unatokana na sheria zetu, kwa maana ya Katiba na Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32,” amesema.

Ameongeza kuwa,suala la uhalali wa Tume hiyo halipaswi kuwa na mjadala mkubwa kwa kuwa msingi wake umejengwa katika mamlaka ya kikatiba na kisheria aliyopewa Rais.

MAJAJI WA RUFAA WAPEWA SIFA

Wakili Nkuba pia amezungumzia sifa na uadilifu wa wajumbe walioteuliwa katika Tume hiyo, akisema sehemu kubwa ya wajumbe ni majaji wenye uzoefu mkubwa katika utoaji wa haki.
Amesema,uwepo wa majaji kutoka Mahakama ya Rufani unaongeza imani kwamba Tume hiyo inaweza kufanya kazi kwa weledi, usawa na haki, kwa kuwa Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya juu zaidi ya utoaji haki nchini.

Aidha, amesema uamuzi wa kuwahusisha majaji kutoka mataifa mengine yakiwamo Uganda na Namibia, unaendana na misingi ya sheria inayozingatia umuhimu wa mtu kutokuwa mwamuzi katika jambo ambalo linaweza kumhusisha moja kwa moja.

Akitumia kanuni ya kisheria nemo judex in causa sua, Wakili Nkuba amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kuondoa uwezekano wa mgongano wa maslahi na kuongeza uaminifu katika mchakato wa uchunguzi.

Kwa maelezo yake, kwa kuwa Tume ya Jaji Lila inachunguza matukio ya jinai yanayoweza kuwahusisha watu au taasisi mbalimbali, ushiriki wa wajumbe kutoka nje unaweza kusaidia kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa mtazamo huru na usioegemea upande wowote.

TOFAUTI KATI YA TUME YA CHANDE NA LILA

Wakili Nkuba amesisitiza kuwa,pamoja na Tume zote mbili kuhusisha matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, zina hadidu za rejea na malengo tofauti.

Amesema,Tume iliyoongozwa na Jaji Chande ilikuwa na jukumu pana la kuchunguza chanzo, sababu na madhara ya ghasia hizo, pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto zilizobainika.

Kwa upande mwingine, amesema Tume ya Jaji Lila imepewa jukumu maalumu la kuchunguza matukio ya kijinai yaliyotokea, kubaini waliohusika na kuweka wazi namna ambavyo watu au taasisi mbalimbali zilishiriki katika matukio hayo.
“Tume ya Jaji Lila iko very specific,yenyewe inakwenda kuchunguza matukio ya kijinai, kwa maana kwamba kazi kubwa imefanywa na Tume ya Jaji Chande ya kuangalia sasa chanzo na madhara, lakini ikagundua kwamba kuna watu ambao walishiriki au kuna vyombo ambavyo vilishiriki kudhamini, kufadhili au kuchochea,”amesema.

Amefafanua kuwa,Tume mpya inalenga kwenda hatua nyingine kwa kuchunguza kwa kina matukio hayo na kubaini nani anawajibika kwa matukio mahususi yaliyotokea.

“Kwa hiyo inakwenda sasa kuangalia nani anawajibika katika lipi, ili waliohusika na kudhamini au kufadhili au kushiriki waweze kuwajibika,”amesema.

WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO

Wakili Nkuba ametoa wito kwa wananchi na wadau wote wenye taarifa kuhusu matukio yanayochunguzwa kutoa ushirikiano kwa Tume hiyo ili iweze kubaini ukweli na kufikia hitimisho linalozingatia ushahidi.

Amesema,kwa mujibu wa sheria, Tume ya Uchunguzi ina uwezo wa kuomba ushahidi, nyaraka na taarifa kutoka kwa watu mbalimbali pale inapobainika kuwa taarifa hizo zinaweza kusaidia katika uchunguzi.

Kwa hiyo, amesema wananchi wenye taarifa muhimu kuhusu matukio ya ghasia, waliohusika,waliofadhili,waliodhamini au kuchochea matukio hayo wanapaswa kutumia fursa hiyo kuwasilisha taarifa zao kwa Tume.

Amesema,ushirikiano huo ni muhimu kwa sababu lengo la uchunguzi si kumuonea au kumhukumu mtu, bali kubaini ukweli kuhusu matukio yaliyotokea na kuweka wazi uwajibikaji wa wahusika kwa mujibu wa sheria.
Wakili Nkuba amesisitiza kuwa,Tume hizo mbili zinapaswa kutazamwa kwa kuzingatia tofauti za hadidu zao za rejea na madhumuni yake, badala ya kuzichukulia kama taasisi zinazofanya kazi zinazofanana.

Amesema, kwa kufanya hivyo, jamii itaweza kuelewa kwamba Tume ya Jaji Chande ililenga zaidi kuchunguza chanzo na madhara ya ghasia na kutoa mapendekezo, wakati Tume ya Jaji Lila inalenga zaidi kuchunguza matukio ya jinai na kubaini wahusika.

Vilevile, Wakili Nkuba ametoa wito kwa wananchi kuacha dhana na tuhuma zisizo na ushahidi, badala yake kutoa taarifa na ushahidi kwa chombo hicho ili ukweli uweze kubainika kwa mujibu wa sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here