Ufilipino yawaokoa raia wake ambao walikuwa wanatumbukia katika usafirishaji haramu wa binadamu na ajira za ulaghai

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA nchini Ufilipino zimewazuia abiria wanane waliokuwa wakielekea Indonesia baada ya kubaini viashiria kwamba huenda walikuwa wameandaliwa kusafirishwa kwa ajili ya ajira kwa njia za udanganyifu, katika kile kinachodaiwa kuwa ni mbinu ya uhalifu inayojulikana kama “catphishing”.
Hatua hiyo imechukuliwa katika kuendeleza maagizo ya Rais Ferdinand Romualdez Marcos Jr. ya kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu na ajira za ulaghai zinazowalenga Wafilipino wanaotafuta fursa za kazi nje ya nchi.

Abiria hao, wenye umri kati ya miaka 26 na 49, walikuwa wanaume watano na wanawake watatu.

Kwa pamoja walikamatwa Agosti 7 katika Kituo cha Kwanza cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ninoy Aquino, walipokuwa wakijiandaa kusafiri kwenda Surabaya, Indonesia kupitia Malaysia.

Awali, abiria hao waliwaeleza maofisa kwamba walikuwa wakielekea Indonesia kwa ajili ya mapumziko ya siku tano.

Pia walidai kuwa, walikuwa wakisafiri pamoja na baadhi ya watu waliowahi kufanya nao kazi katika kituo cha huduma kwa wateja (call center) mjini Makati.

Hata hivyo, wakati wa mahojiano ya kina, maofisa walibaini kutokubaliana katika maelezo yao.

Miongoni mwa mambo yaliyozua mashaka ni kutowafahamu vizuri baadhi ya watu waliodai kuwa ni wenzao katika safari hiyo.

Uchunguzi zaidi ulifichua kwamba safari hiyo huenda haikuwa ya mapumziko kama walivyodai awali.

Kwa mujibu wa mamlaka, abiria hao walikuwa wamealikwa kwenda kufanya kazi Indonesia kama mawakala wa huduma kwa wateja, baada ya kuahidiwa mishahara ya kati ya dola za Marekani 1,000 na 1,500 kwa mwezi.

Hofu zaidi iliibuka baada ya maofisa wa uhamiaji kubaini kwamba watano kati ya abiria hao waliwahi kufanya kazi nchini Cambodia na Myanmar, mataifa ambayo yamekuwa yakihusishwa na visa vya ulaghai wa ajira na usafirishaji haramu wa wafanyakazi.

Mamlaka pia zilibaini kuwa wawili kati yao waliripotiwa kuondoka katika nchi hizo kupitia njia zisizo rasmi, maarufu kama “backdoor routes”.

Mmoja wa abiria hao alikuwa amewahi kurejeshwa nchini Ufilipino kutoka Myanmar baada ya kuripotiwa kuwa mwathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu.

Mwingine amewahi kufanya kazi ya ualimu nchini Thailand, licha ya kuwa na hadhi ya kuingia nchini humo kama mtalii pekee.

Maelezo hayo yameongeza uzito wa mashaka kwamba kundi hilo huenda lilikuwa katika hatari ya kuangukia tena katika mtandao wa usafirishaji haramu wa watu au ajira za ulaghai.

Kamishna wa Uhamiaji wa Ufilipino, Joel Anthony Viado amesema,tukio hilo linaonesha kuwa mbinu ya “catphishing” bado inatumika na inaendelea kuwaweka Wafilipino katika hatari, hasa wale wanaovutiwa na ahadi za ajira zenye mishahara mikubwa nje ya nchi.

Viado amesema, kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba baadhi ya watu waliokutwa katika kundi hilo tayari walikuwa wamewahi kukumbana na mazingira ya unyonyaji nje ya nchi, kuokolewa au kurejeshwa nchini, lakini baadaye wakajikuta wakivutwa tena kwenye mpango mwingine unaoweza kuwa hatari.

Kwa mujibu wa Viado, wahalifu wanaendelea kubadilisha mbinu zao, lakini msingi wa ulaghai huo unabaki uleule kutoa ofa zinazovutia za ajira, kuahidi mishahara mikubwa na kujenga simulizi zinazolenga kupata imani ya waathiriwa.

Amesisitiza umuhimu wa waombaji kazi kuthibitisha kwa kina ajira wanazopewa kabla ya kusafiri nje ya nchi, ikiwemo kuhakiki uhalali wa kazi yenyewe, mwajiri, wakala anayehusika pamoja na nyaraka zote za ajira na safari.

Baada ya kuzuiwa, abiria hao walikabidhiwa kwa Baraza la Mashirika Mbalimbali la Serikali la Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu (Inter-Agency Council Against Trafficking-IACAT) kwa ajili ya kufanyiwa tathmini, kupewa msaada na kuchukuliwa hatua stahiki.

Mamlaka zinawachukulia kama watu wanaoweza kuwa waathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu na ajira za ulaghai, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira halisi ya safari yao na mtandao uliokuwa nyuma ya ofa hizo za ajira.

Tukio hilo limeibua tena tahadhari kwa wanaotafuta ajira nje ya nchi kuhusu hatari ya kuamini ofa zinazotolewa kupitia mawasiliano ya mtandaoni au watu wasiojulikana bila kufanya uhakiki wa kina.

Mamlaka ya Uhamiaji imewataka wasafiri kutotegemea ahadi zinazotolewa na watu wanaowasiliana nao mtandaoni au mawakala wasio na uthibitisho wa kisheria.

Badala yake, wanatakiwa kutumia njia rasmi za serikali kuthibitisha uhalali wa mwajiri, nafasi ya kazi na nyaraka husika kabla ya kuondoka nchini.

Kwa mamlaka, tahadhari hiyo ni muhimu zaidi kutokana na namna mitandao ya usafirishaji haramu wa watu inavyoendelea kubuni mbinu mpya za kuwafikia waathiriwa, huku ikitumia ahadi za mishahara mizuri na maisha bora kama chambo cha kuwavuta wanaotafuta ajira nje ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here