GEITA-Naibu Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mafanikio ya mpango wake wa ununuzi wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini, akisema mpango huo umechangia kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini.
Dkt.Kiruswa ametoa pongezi hizo leo Septemba 27,2026 alipotembelea banda la Benki Kuu katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.
“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya. Muda si mrefu, Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa ya dhahabu, ambayo ni mbadala wa fedha za kigeni,”amesema Dkt.Kiruswa.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Naibu Waziri huyo katika banda la Benki Kuu, Meneja Mawasiliano, Bi. Victoria Msina amesema, hadi sasa BoT imenunua jumla ya tani 34.7 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini.
Bi. Msina ameongeza kuwa,mafanikio ya mpango huo yamevutia nchi mbalimbali za Afrika kuja Tanzania kujifunza na kupata uzoefu kuhusu utekelezaji wa mpango wa ununuzi wa dhahabu, zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Msumbiji na Eswatini.
Kwa upande wake, Mchambuzi wa Masuala ya Fedha, Bi. Gloria Maembe amesema, mpango wa ununuzi wa dhahabu una mchango mkubwa katika kuongeza akiba ya fedha za kigeni nchini.
“Akiba ya fedha za kigeni imefikia Dola za Marekani bilioni 6.03, ambapo Dola za Marekani bilioni 2.05 zimetokana na dhahabu,”amesema Bi.Maembe.
Ushiriki wa Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini ni sehemu ya mikakati yake ya kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, sera na shughuli mbalimbali inazotekeleza katika kuimarisha uchumi wa taifa.
Maonesho hayo yanayofanyika kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 3,2026 yanaongozwa na kaulimbiu “Madini ni utajiri, tuwajibike kwa pamoja kufikia Dira ya Taifa 2050.”
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
Dhahabu
Dr Steven Kiruswa
Habari
Ununuzi wa Dhahabu
Uwekezaji Sekta ya Madini




