ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar inaendelea kupiga hatua katika sekta za uwekezaji na utalii, hali inayozidi kuimarisha nafasi ya Zanzibar katika soko la utalii duniani.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Septemba 6,2026,wakati akizindua hoteli za Anaya Hotels & Resorts Zanzibar na Kappa Senses Zanzibar, zilizopo Pwani Mchangani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesema uwekezaji katika hoteli hizo umefikia zaidi ya Dola za Marekani milioni 52, huku miradi hiyo ikiwa tayari imezalisha ajira 371 kwa wananchi.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar sasa inapokea zaidi ya watalii laki moja kwa mwezi, hatua inayoongeza matumaini ya kufikia lengo la kupokea watalii milioni moja kwa mwaka.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utalii jumuishi unaomnufaisha mwekezaji, mtalii na mwananchi, ikiwemo kuhakikisha hoteli zinatumia bidhaa zinazozalishwa nchini na kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wasanii wa sanaa za mikono kuuza bidhaa zao.
Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi, kuboresha miundombinu na kutoa ushirikiano unaohitajika ili kukuza zaidi uwekezaji na utalii kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Tags
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Habari
Hoteli za Kisasa Zanzibar
Hoteli za Kitalii
Hoteli za Kitalii Zanzibar
Sekta ya Utalii Zanzibar
Zanzibar News

















