Rais Dkt.Samia kuzindua miradi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua majengo ya Ofisi za Wizara, Taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika Septemba 8,2026 katika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya Mji wa Serikali Mtumba.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi ameyasema hayo leo Septemba 6,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo.

Amesema,uzinduzi huo utahusisha maeneo matatu makuu ambayo ni majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi 11 za Serikali na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.

Profesa Kabudi amesema,kukamilika kwa majengo hayo, kutawezesha watumishi 18,510 kutumia ofisi za Mji wa Serikali Mtumba.

“Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za muda,ujenzi wa majengo hayo ulianza Novemba 28, mwaka 2018 na kukamilika Machi 22 mwaka 2019, hatua iliyowezesha baadhi ya watumishi wa wizara na taasisi kuanza kuhamia.
"Awamu ya pili ya ujenzi ilianza Oktoba,2021 ikiwa inalenga kujenga majengo ya kudumu kwa ajili ya watumishi wote wa wizara na taasisi zilizopangwa kuhamia Mtumba.Pia ilihusisha ujenzi wa miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo barabara za lami."

Profesa Kabudi amesema,mbali na barabara hizo, miundombinu ya kudumu ya mawasiliano pamoja na Uwanja wa Mashujaa imekamilika na itakuwa sehemu ya miundombinu itakayotumika katika shughuli za Serikali.

Hata hivyo, amesema baadhi ya miradi bado iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umeme inayopita chini ya ardhi yenye urefu wa kilomita 42.
"Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na uondoshaji wa maji taka, TEHAMA,ufungaji wa mifumo ya usalama ya CCTV Camera, ujenzi wa kituo cha zimamoto pamoja na utekelezaji wa mpango wa upandaji miti na ustawishaji wa Mji wa Serikali nazo zinafanyika,"amesema.

Amesema,Rais Dkt.Samia ameendelea kuweka msisitizo katika kuboresha mazingira hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani za Wizara na taasisi 26 zinazohamia katika majengo hayo.

Profesa Kabudi amesema,hatua hizo zinaendelea kuufanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa alama muhimu za utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.
Amesema, uwekezaji huo pia unatarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here