NA GODFREY NNKO
OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria na kanuni, uwazi, ushindani wa haki na matumizi yenye tija ya fedha za umma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Msisitizo huo umetolewa leo Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa OTR, Bw. Sabato Kosuri wakati akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina katika kikao kazi kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), wahariri na waandishi wa habari.Kikao kazi hicho, kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kuzipa taasisi na mashirika inayoyasimamia kueleza kwa kina kuhusu mambo wanayoyafanya ili wamiliki wa taasisi hizo ambao ni Watanzania waweze kufahamu zilipotoka, zilipo na zinapoelekea.
Bw. Kosuri amesema, PPRA ni taasisi muhimu katika usimamizi na udhibiti wa mifumo ya ununuzi wa umma, inayosaidia kuhakikisha kuwa taratibu za manunuzi katika taasisi na mashirika ya umma zinafanyika kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, uwazi na ushindani, huku thamani halisi ya fedha zinazotumika ikipatikana.
Ameeleza kuwa, OTR ina jukumu la kusimamia taasisi na mashirika ya umma, hivyo usimamizi madhubuti wa matumizi ya rasilimali za Serikali, hususan katika eneo la ununuzi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Kwa msingi huo, PPRA ni mshirika muhimu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kuhakikisha ununuzi wa umma unafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zinazolinda maslahi ya umma,” amesema Bw. Kosuri.
Ameongeza kuwa, ununuzi wa umma ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, utoaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa miundombinu, hivyo namna unavyosimamiwa ina athari za moja kwa moja katika matumizi ya rasilimali za Serikali na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Pia, amesema kuwa, utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya PPRA unaweza kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, kupitia kuimarisha utawala bora, kupunguza upotevu wa rasilimali, kuongeza uwajibikaji na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.
Bw. Sabato amebainisha kuwa, mifumo bora ya ununuzi wa umma inaweza pia kufungua fursa zaidi kwa wazalishaji, wajasiriamali na wafanyabiashara wa Kitanzania, hatua inayoweza kuchochea ukuaji wa viwanda, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa ndani.
Akizungumzia umuhimu wa kikao kazi hicho, Bw. Kosuri amesema, jukwaa la kukutanisha taasisi za umma na vyombo vya habari linatoa nafasi ya kujadiliana, kubadilishana mawazo na kupata maoni yatakayosaidia kuboresha utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.
Vilevile amesema, ushirikiano kati ya taasisi hizo na vyombo vya habari ni muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na uwazi, huku ukitoa fursa kwa wahariri na waandishi wa habari kutoa ushauri kuhusu maeneo yanayohitaji maboresho.
Bw. Kosuri ameeleza kuwa, maoni na mapendekezo yanayotolewa kupitia majadiliano hayo yanaweza kusaidia kuimarisha utendaji wa taasisi za umma na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mbali na hayo, amesisitiza kuwa, ushirikiano endelevu kati ya OTR, PPRA na vyombo vya habari ni muhimu katika kujenga uelewa mpana kuhusu majukumu ya taasisi hizo na kuhamasisha usimamizi wenye tija wa rasilimali za umma.
Tags
Dar es Salaam
Dira ya Taifa 2050
Habari
Habari za Uchumi
Ofisi ya Msajili wa Hazina
OTR
PPRA
Rasilimali za Umma
Sabato Kosuri
Ununuzi wa Umma
