Waziri Mhagama:Timu ya wataalam imeundwa kuainisha mapungufu ya OPRAS na kupendekeza mfumo mpya utakaoongeza uwajibikaji

NA JAMES K.MWANAMYOTO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake imeunda kikosi kazi maalum cha wataalam wabobezi kinachoendelea kufanya mapitio na kuainisha mapungufu yote ambayo yamejitokeza kwenye Mfumo wa Wazi wa Upimaji wa Utendaji Kazi wa watumishi (OPRAS) ili kupendekeza mfumo mpya wa kielektroniki wa wazi na rafiki ambao utaondoa upendeleo, udanganyifu na kuongeza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza nao kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Akizungumza na Watumishi wa Umma kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma, Mhe. Jenista amesema, ofisi yake imechukua hatua hiyo ya haraka kuunda kikao kazi hicho ili kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye azma yake ni kuwa na mfumo bora wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma tofauti na mfumo wa OPRAS uliopo hivi sasa, ambao umebainika kuwa na mapungufu ambayo hayatoi matokeo halisi ya utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja.

“Katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais, Ofisi yangu imeamua kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kuunda timu hii maalum ya wataalam wabobezi ili kuhakikisha tunapata mfumo bora, imara na wenye tija ambao utaondoa changamoto za utekelezaji zilizojitokeza katika mfumo wa OPRAS unaotumika hivi sasa, uliosanifiwa mwaka 2004,” Mhe. Jenista amefafanua.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Umma kupitia vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu uboreshaji wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, timu hiyo ya wataalam imemthibitishia kuwa, mfumo huo mpya wa kielektroniki wa upimaji wa utendaji kazi wa mtumishi mmoja mmoja unaopendekezwa utakuwa ni mfumo rafiki na wenye manufaa kwa Watumishi wa Umma, ambao utarahisisha uandaaji wa mikataba ya utendaji kazi na kutoa fursa ya kujiwekea malengo na shabaha kwa kila mtumishi.

“Mfumo huo mpya utapunguza muda wa Watumishi wa Umma kucheza na makaratasi na utawataka viongozi wenye dhamana ya usimamizi wa watumishi kutimiza wajibu wao kwa kufanya ufuatiliaji, kupima na kutoa mrejesho wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma bila kuwaonea, kuwakandamiza ama kutumia hila ya aina yoyote,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imejipanga kuhakikisha mfumo huo mpya wa upimaji wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma uanze kutumika rasmi tarehe 01 Julai, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news